BURIANI KEN WALIBORA

BURIANI KEN WALIBORA

Na HUSSEIN M KASSIM

Kama ni machozi, basi yanitoka kapakapa

Kama ni jitimai, sonono haliniishi

Mawazo na fikra? Ni mkururo baada ya mwingine.

 

Tanzia ya kifo chake baba Kennedy Atanasi Waliaula niliipokea mkesha wa tarehe 15/04/2020. Hapana shaka kuwa nitaikumbuka tarehe hii milele. Namwita baba kwa maana halisi ya mzazi. Ameniathiri pakubwa mno na pia watu wengine nchini Kenya na duniani kote. Ametuchochea baadhi yetu kufanya mambo makubwa makubwa bila shaka. Ama sio ubaba huu?

Nilikumbana na bingwa huyu kwa mara ya kwanza kupitia kitabu chake, Ndoto ya Amerika. Nilikuwa katika darasa la nne wakati huo. Weledi wake wa kifasihi katika kitabu hicho ndio uliozitekenya na kuzichochea hisia za kutaka kuwa mwandishi. Na ndicho kiini hasa naandika mpaka sasa. Ken ndiye chemchemi ya mahaba yangu ya utunzi, uandishi, fasihi na zaidi ya yote, mapenzi ya kiswahili.

Kupitia vitabu vyake vingine kama vile ndoto ya Almasi, Kufa Kuzikana na Siku Njema, moto wa kutaka kuwa bora zaidi uliendelea kuchochewa katika nafsi yangu.

Nimeishi kumsifu Ken Walibora kwa utunzi wake usio mgumu kueleweka. Daima, humtia msomaji wake kwenye ngalawa ya simulizi, akamburudisha na kumwongoa kwa lugha tamu na nyepesi hadi tamati. Ameacha pengo! Hakika, ameliacha pengo kubwa mno.

Buriani Ken wetu. Buriani bingwa. Buriani shupavu wewe mwenye staha. Buriani kielelezo changu. Buriani kielelezo chetu. Buriani mtangazaji mahiri. Buriani kwa kitengo chako katika Gazeti la Taifa Leo. Buriani baba. Buriani. Umetuwacha na ukiwa. Tunakupeza tayari. Tutakupeza daima. Tutakupeza Walibora.

Hakika umeiacha dunia ikiwa bora kuliko ulivyoipata. Umeiwacha bora zaidi aisee! Umeiwacha bora kwa kunifaa mimi. Umeiwacha bora kwa kutufaa sisi, wao na wengine. Umeiwacha bora kwa kuilisha fasihi yako komavu, taanusi, yenye ukwasi na faafu. Fasihi isiyokufa abadan! Fasihi isiyolegea. Fasihi, kiungo madhubuti cha urazini wa jamii. Lala salama. Pumzika vyema mkuu.

 

SALAMA WALIAULA

Umetoweka mhimili, wa’ndishi twataabika

Twasononeka kwa hili, baba yetu kaondoka

Ameng’atwa na ajali, maisha yakakatika

Kuno kustahimili, jamani ninaponzeka

 

Lala salama mwalimu, kwa dhati tunakupenda

Umetujaza fahamu, makini yametuganda

Fasihi twaiheshimu, tutazidi kuiponda

Nenda salama mwalimu, mbegu umeshaipanda

 

 

Suggested reads:

10 thoughts on “BURIANI KEN WALIBORA”

  1. Mimi nasonasona kwa kilio hadi wa leo.Nimeshindwa kabisa hata kubuni shairi la kumwaga Galacha huyu. Nitatumia maneno yapi kumsifu? Yapi? Lipi nitaandika liweke wazi mapenzi yangu na bingwa huyu? Bingwa niliyeondokea kumfahamu kupitia kazi take ya CHAPUCHAPU nikiwa darasa la nne!

    Taandika nini kieleze alivyonipa msawazo wa kuandika? Dah! Kifo! kifo! kifo! Ni juzi tu E.Kezilabi umetupoka Leo tena!

    Buriani bingwa! Nitatangamana nawe kupitia maandishi yako.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Open chat
1
Need help?
Writers Guild Kenya
Hello.
How can we help you?