Tangu utotoni mwangu mwendazake babu yangu alikuwa na mazoea ya kunighania ngano haswa kuhusu Maumau. Wakati mwingine nilimfuata hadi kwenye mikahawa ya uchwarauchwara kule kijijini kwa lengo la kusoma gazeti la Taifa Leo, yeye akidhania kuwa hamu yangu ni chai na andazi ambazo ziliuzwa kwa sh.10 pekee, kumbe mwito mkuu ulikuwa maandishi. Nilipenda vitabu na magazeti kweli. Nikilala ama kwenda shambani sikosi kitabu. Tangu hapo nikatamani kuwa mwandishi.
Nilipatana na Mhesh. Gabrieli nilipokuwa mwanafuzi katika chuo kikuu cha Masinde Muliro mwaka wa 2014. Mlikuwa na kongamano la vijana kule Kakamega ambalo mgeni wa heshima katika siku hiyo alikuwa Prof. Ken Walibora (sifai kumtanguliza bingwa huyu). Kwa wakati ule nilikuwa nimejiandaa kuwakabidhi wawili hawa muswada niliokuwa nao- fuata ndoto yako.
WGK ilikuwa inaanza kukita mizizi mle chuoni chini ya mwakilishi, Frank Omondi. Nilipomwomba Mhesh. Gabrieli nafasi ya kuzungumza naye hakunipinga. Basi nikamfungulia roho naye akawa tayari kunisikiliza kwa ahadi kuwa angenipatia jawabu baada ya muswada wangu kuhaririwa. Kwa upande mwingine nakumbuka nilivyomfuata Prof. Ken hadi hadi kwa lango la gari lake alipokuwa akiondoka. Mvua iliyokuwa ikinyesha haikutupatia muda mwingi pamoja japo aliniahidi kunipatia jibu baada ya siku fulani. Nami nikatulia tuli na kuingoja siku yangu, siku ambayo ningepitishwa kuwa mwandishi!
Baada ya takribani miezi mitatu Mhesh. Gabrieli aliniarifu kuwa mhariri wangu, Winnie Ogenche, alikuwa ameukataa muswada wangu kwa misingi tofauti ambayo nilipata ripoti yake. Moyo wangu karibu utamauke kwa kufifia kwa ndoto yangu. Niliona kuwa lengo la kuwa mwandishi lilikuwa fikira tu ambayo haikuwa na msingi wowote kwangu na kudhania kuwa ningechapishwa ni jambo ambalo sikuridhiwa maishani.
Mojawapo ya maswala niliyofaa kurekebisha ilikuwa mada ya mswada. Katika hali hii ya kutamauka binti mmoja rafiki yangu alinishawishi kuendelea na ndoto yangu kwa kunikabidhi jezi iliyoandikwa “Just do it.” Tangu hapo nikaamua ima fa ima, sikosi kukazana hadi nichapishwe. Isitoshe, siwasahau afisa mtendaji, WGK na kiongozi wa wanafunzi MMUST, Daudi Kemboi kwa kuniamini. Basi nikajikita katika utafiti na kujinyima kwa lengo la kuurekebisha muswada, hamu kuu ikiwa kuwapa motisha wanaokata tamaa maishani pamoja na watu walio na ndoto kubwa maishani.
Ipo Siku ni riwaya ya kipekee inayounganisha maudhui mbalimbali kote duniani ili kueleza maswala ibuka kwa njia ya burudani na kuelimisha. Utapatana na wahusika wakuu, Jabali na Bahati, ambao japo kila hali inaenda kinyume na matarajio yao wawili hao hawafi moyo. Kwao, changamoto ni nafasi murua ya kupaa angani kama ndege. Ufisadi na wivu ni maudhui mengine yaliyotajwa kwa kiwango fulani. Ni kitabu kinachoendelea kujikita mizizi hapa nchini.
Nina imani kuwa siku moja kitavuka mipaka ya Kenya-ipo siku. Hakika, bila Mhesh. Gabrieli na familia ya WGK safari hii haingekamilika. Huyu bwana alikuwa mgeni kwangu kabisa ila kujitolea kwake ungedhani tulikuwa ndugu wa tumbo moja! Ni mengi aliyonifanyia ambayo kuyasahau nitakuwa mtovu wa nidhamu na mkosa wa shukrani.
Kumbe kuandika kitabu kunahitaji kujiamini, nidhamu ya wakati, kuzungukwa na marafiki wanaoamini bidii yako (huenda akuwe mmoja ila mwamini tu), na kutanguliza imani mbele. Bila shaka hakuna lisilowezekana. Wanaootea siku hakika siku yao inafika. Asiyeotea siku hana siku. Ipo Siku. Inshallah!
Solomon Muya ndiye Mwandishi wa Riwaya ya ‘Ipo Siku’ ambayo imechapishwa na Writers Guild Kenya.
Riwaya hii ndiyo Writers Guild Book Club – Book of the month.