SAUTI YA KEN WALIBORA

SAUTI YA KEN WALIBORA

NA EDWARD OMBUI

Ukitazama kwa jicho la ndani utagundua kuwa chembechembe za tawasifu ya Ken Walibora zinajitokeza katika Siku Njema (1996), Ndoto Ya Amerika (2001), Kufa Kuzikana (2006), Ndoto Ya Almasi (2012), Kidagaa Kimemwozea (2012) na vitabu vingine vyake.

Msanifu Kombo ndilo jina lake, lakini jina la kupanga la mhusika mkuu katika riwaya ya Siku Njema ni Kongowea, na si Kongowea tu, bali ‘Kongowea Mswahili. Ni jina alilopewa kutokana na jinsi alivyokiona Kiswahili na kukienzi kama mboni ya jicho lake. Mhusika anampalia mama yake sifa sufufu kwa kumzaa, kumlea na kumsaidia kupata elimu ya vitabu na ya maisha.

Msanifu Kombo Almaarufu Kongowea Mswahili anasimulia juu ya aushi yake. Yeye alizaliwa mjini Tanga. Wakati huo, mamake kwa jina Zainabu Makame, mwimbaji hodari wa Taarab alikuwa maarufu sana. Sifa zake za uimbaji zilikuwa zimeenea ndani na nje ya Tanzania kama moto katika kichaka kikavu. Awali maisha ya Kongowea Mswahili yalikuwa mazuri. Halafu maisha yake yanachukua mkondo mpya baada ya mamake kuugua ugonjwa usio na jina wala dawa. Mkaza-mjomba hampendi Kongowea kwa kuwa yeye ni mwerevu kuliko watoto wake. Umaarufu wa huyu mhusika unapanda kiwango kingine anaposhinda katika mashindano ya uandishi mkoani Tanga. Kongowea anaupasi mtihani ila anakosa karo. Kwa hivyo, masomo yake yanafikia hatma ya ghafla. Sasa analazimika kufanya kazi ya useremala ili kujikimu. Wakati huu wazo la kutaka kujua ni nani babake linamjia. Mawazo haya yanapozidi, anaamua kufunga safari ya kwenda nchini Kenya haswa Kitale- Magharibi ya Kenya kumtafuta babake.

Anapofika Kitale, hafanikiwi kumpata babake papo kwa hapo. Lakini hakati tamaa. Bi Mercy, mkulima maarufu huko Kitale anampa kazi. Hili linamwezesha kujikimu huku akimtafuta babake mzazi. Katika hamsini zake, anafahamiana na Mzee Kazikwisha anayeaminiwa kuwa ni kichaa. Hatimaye Kongowea Mswahili anakuja kugundua kuwa mzee huyo ndiye baba yake, Juma Mukosi. Mzee huyo anamtambua mtoto wake mara tu anapomwona lakini hajitambulishi mpaka dakika yake ya mwisho ya uhai wake. Kabla ya Mzwe Kazikwisha (Juma Mukosi) kuaga, anaamua kumfichulia Kongowea Mswahili kila kitu kupitia barua. Hata hivyo, babake anamwachia mali chekwachekwa ambayo hata yakichotwa hayawezi yakaisha. Maisha ya maskini Msanifu Kombo yakabadilika. Akawa mkwasi wa kutajika. Baadaye anamuoa Vumilia, rafikiye wa utotoni na kuishi Raha mustarehe.

×××

Katika ‘Nasikia Sauti ya Mama‘ Ken Walibora amesawiriwa kama mchoraji hodari mwenye kipawa cha aina yake. Riwaya hii inaeleza kuhusu maisha ya utotoni ya Ken Walibora. Mwandishi anaeleza jinsi alivyojifunga kibwebwe huku akifanya bidii na juhudi zaidi ya mchwa wajengao vichuguu kwa mate kuhakikisha kwamba amefaulu. Na ni ukweli kwamba bidii yake ilizaa matunda na ilidhihirika kwa namna alivyokuwa anakitumia Kiswahili kwa ufasaha, madaha, madoido na umufti usio kifani. Kila mara Ken Walibora aliposimama kuzungumza ungedhani kwamba punde tu alipozaliwa, malaika Jibrili alikuja akaupaka ufizi wake wote Kiswahili na kuweka matamshi ya kiada katika mazungumzo yake.

Guru Wallah Bin Wallah alisema hivi katika mojawapo ya mahojiana yake;

Ukitaka kuvuna mavuno ya siku moja, panda uyoga. Utauvuna, ule siku hiyohiyo na hata pengine uoze siku hiyohiyo. Ukitaka mavuno ya miezi miwili, panda miharagwe. Ukitaka mavuno ya miezi sita, panda mihindi. Ukitaka mavuno ya mwaka mmoja, panda mitunda. Lakini ukitaka mavuno ya kudumu, ya kila siku na kila wakati, popote ulipo bila kumaliza hadi Kufa, basi nenda ukapande mbegu ya elimu. Hapa ndipo utakapovuna milele na milele, daima dawamu.”

Nimemnukuu Guru kwa sababu hii, sote tunajua kwamba kati ya sifa nyingi za Ken Walibora ni kwamba alikuwa msomi. Alikuwa mtafiti mkubwa wa lugha ya Kiswahili. Alijua dhahiri kwamba elimu huhitaji utafiti wala si utafishi. Watafiti ndio wapatao ukweli wa mambo lakini watafishi huzua tafrani, tafashi na mtafaruku. Na katika elimu vitu hivi havitakikani kwani havitafikisha watu katika kuelewa, kuerevuka na kutaalamika kidedea. Aliitafuta elimu kwa uvumilivu kwa kutumia vitabu mufti. Kutoka kushika kilelecha cha mkia darasani hadi kuwa profesa inadhihirisha bidii yake ilizaa matunda.

Katika kitabu changu cha ‘Mwangwi Wa Maisha’ Diwani ya Mashairi, ninasema hivi;

Safari huanza kwa hatua moja. Nayo hatua ndogo ni kubwa. Safari ya maisha ni ngumu. Kuna kusonga mbele na kuanguka pia. Miiba ya sumu itakudunga na viatu kuisha soli. Utapita kwenye misitu mirefu na kutishiwa na wanyamapori. Utazama na kuelea kwenye bahari zenye vina virefu lakini usitishike. Kusafiri ni lazima, liwe lolote litakalokuwa lije lolote litakalokuja.”

Riwayani ‘Nasikia Sauti Ya Mama’ Walibora anakiri kwamba kichocheo chake kikuu katika kufikia ufanisi wake ni mama yake. Uelekezi wa mama yake ulikuwa ni dawa mjarabu iliyotibu maradhi yaliyomsibu. Kama sio mamake, Ken Walibora Almaarufu Mtoto Wa Mwalimu ni nani ila udongo usio na sura yoyote ya chombo. Mamake alikuwa mfinyanzi aliyemfinyanga mtoto wake hadi akawa ‘mtu’.

‘Nasikia Sauti Ya Mama’ inatuchorea taswira ya tawasifu ya Ken Walibora kutoka utotoni hadi ukubwani. Mumo tunaelezwa changamoto nyingi alizokumbana nazo zikiwemo maradhi, umaskini na zingine nyingi. Vilevile tunaelezwa kuwa Ken Walibora alikuwa shabiki na mchezaji wa kabumbu, mwanariadha na mchoraji hodari.

Baadhi ya vitabu vyake maarufu ni Siku Njema, Kidagaa Kimemwozea, Damu Nyeusi (2013), Kufa Kuzikana, Ndoto Ya Almasi, Kiti Cha Moyoni na hadithi nyingine (2007), Waja Leo; Diwani Ya Mashairi (2012), Nasikia Sauti Ya Mama, Ndoto Ya Amerika.

Diwani yake ya Mashairi Waja Leo inadhihirisha kuwa Marehemu Prof Ken Walibora alikuwa mshairi wa kupigiwa mfano. Lugha iliyotumika katika mashairi yake ina maneno mateule. Na uzuri wa mashairi yake ni uzuri wa milele.

Ninatua kwa kumwandikia shairi Marehemu Prof Ken Walibora ili kumhakikishia huko aliko kwamba vizazi na vizazi havitaacha kuwasherehekea mashujaa kama yeye siku zote.

 

ULAZWE PEMA PEPONI

Yamejaa maozini, majonzi nayo huzuni

Mesononeka moyoni, maraha hapatikani

Sijui nifanye nini, nie mpango wa Manani

Ulazwe pema peponi, ndugu Ken Walibora

Ni dua zetu mwandani, uliko uweni vyema

Akujaalie Manani, kupeze zake neema

Kwa heshima na Imani, ulale pema salama

Ulazwe pema peponi, ndugu Ken Walibora

 

Likuwa mwenye imani, asiye hata kiburi

Siye inda asilani, siku zote mwenye kheri

Ulitenda kwa makini, kwa mtima ninakiri

Ulazwe pema peponi, ndugu Ken Walibora

 

Mengi sina kuyasema, tamati hapa mwishoni

Umetenda mengi mema, hapa kwetu mtaani

Najitoma kwa huruma, kwazo zangu shughulini

Ulazwe pema peponi, ndugu Ken Walibora

 

‘Mwangwi Wa Maisha’ Diwani Ya Mashairi, uk 72

 

Edward Ombui Almaarufu Malenga Mdogo ni mwandishi chipukizi, mshairi na mwanamazingira.

Anasoma Technical University of Mombasa.

Sema naye kupitia

+254717890315

Au

Edwardombui2001@gmail.com


 

Suggested reads:

3 thoughts on “SAUTI YA KEN WALIBORA”

  1. Ahsante Sana The Writers Guild Kenya kwa kuchapisha maoni yangu kumhusu Marehemu Prof Ken Walibora. Ahsante zaidi kwa hii nafasi. Nitazidi kuandika kwa sababu hii.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Open chat
1
Need help?
Writers Guild Kenya
Hello.
How can we help you?