Ukoloni Mamboleo Unadhalilisha Uhuru wa Waafrika

Ukoloni Mamboleo Unadhalilisha Uhuru wa Waafrika

Na Sitati Wasilwa

Nchi za Kiafrika zilipojinyakulia uhuru, Waafrika wengi  walihisi kwamba mifumo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yangewanufaisha.

Pindi tu nchi hizi zilipopata uhuru, mabeberu walijiondoa uongozini lakini bado kulikuwepo na dhana ya ukoloni ukizingatia maswala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Kisiasa, utawala ulibuniwa na kuendeshwa kwa kuiga mfano wa ule wa ukoloni. Kijamii, tamaduni za kizungu zilienziwa. Kiuchumi, mitindo ya utendakazi na maendeleo iliiga ile ya kibeberu. Huu ndio ulikuwa msingi wa ukoloni mamboleo.

Ukoloni mamboleo maana yake ni mitindo inayotumiwa na baadhi za nchi kuzitawala nchi nyinginezo bila utumizi wa nguvu. Baadhi ya mitindo inayotumika ni kama ukuzaji wa tamaduni za kigeni, mikopo, ujenzi wa miundo msingi, ubadhirifu wa rasilimali na biashara isiyo na usawa.

Njia moja ya kubaini kuwa ukoloni mamboleo umekita mizizi ni kwa kutazama hali halisi ya tamaduni. Katika nchi za Kiafrika, tamaduni bado zinazingatiwa kwa njia moja au nyingine.

Lakini kuna baadhi ya tamaduni za kigeni ambazo zinadunisha Uafrika na hivyo basi kueneza kasumba ya ukoloni mamboleo.

Kwa mfano, lugha za kigeni zinaenziwa na Waafrika wengi tu na kuna mtindo potovu kuwa wale wasiojua au kujieleza kwa ufasaha katika lugha hizi wapo nyuma kwa kiwango fulani. Wanakejeliwa kwa vigezo vya ukoloni!

Mbona lugha ya Kiswahili inadharauliwa na baadhi ya Wakenya haswa wale wanaodai kuwa wasomi? Jibu lipo; ratiba za shule za msingi na upili zimebuniwa kwa misingi ya ukoloni! Vipi wanafunzi watakiwe kuzungumza Kiingereza, kwa mfano, siku sita kila wiki ilhali wazungumze Kiswahili siku moja kwenye juma nzima? Mwenda zake Ken Walibora aliikemea kwa vikali sana hulka hii.

Wakoloni walidunisha tamaduni za Kiafrika kwa madai ya kutokua endelevu. Hii ni fikra ya kiupumbavu. Duniani kote hamna tamaduni ambazo ni potovu. Watu na jamii hutofautiana na kuna haja ya kuthamini mila na desturi mbalimbali bila ubaguzi wowote.

Hivi sasa Wachina wanafurika barani Afrika katika ile hali ya mchakato wa siasa na uchumi ya kijografia. Lengo lao kuu ni kueneza tamaduni za Kichina barani Afrika ili taifa lao liwe na usemi mkubwa duniani.

Taasisi za Confucius zimejengwa kote barani Afrika kwa minajili ya kueneza lugha ya Kichina. Hii ni njia mojawapo ya kusambaza ukoloni mamboleo. Jambo la kusikitisha ni kwamba baadhi ya serikali za nchi za Kiafrika zina mipango kabambe kujumuisha lugha ya Kichina katika mtaala wa elimu. Mifano ni serikali za Kenya na Uganda.

Majina ya kigeni wanayopewa watoto wakizaliwa ni kioo cha ukoloni mamboleo. La kushangaza pakubwa siku hizi ni hulka ya kuwapa watoto majina ya kizungu kwa misingi ya kumaliza ukabila! Kwa mfano, ‘Tony Roberts’, ‘Faith Blessing’ na mengineyo. Majina hayamalizi ukabila ila fikra na matendo yetu! Majina ya Kiafrika hayana kasoro yoyote. Tuyaenzi.

 

Vipi sanaa ya kigeni kuenziwa ilhali ya Kiafrika kudunishwa? Vipi vyakula vya kigeni kudhaniwa kuwa vizuri kuliko vile vya asili ya Kiafrika? Vipi dini za Kiafrika kudunishwa ilhali za kigeni kukumbatiwa? Vipi harusi za Kiafrika kudhalilishwa ilhali za Kizungu kuenziwa?

Mitaala ya elimu katika nchi mbalimbali barani Afrika imebuniwa kwa misingi ya ukoloni. Hii ndio sababu kuu ya kutokua na suluhisho mwafaka kukabiliana na changamoto zinazowakumba Waafrika.

Mfano bora ni mtaala wa kozi ya uchumi ambao unaelekezwa kwa dhana ya uzungu na hauzingatii fani mbalimbali ya uchumi wa Afrika tangu zama zile. Swala la Kiafrika linalozingatiwa pakubwa na mtaala huu ni maendeleo duni barani ambapo si kweli kwani haipaswi kutumia vigezo fulani kutathmini hali ya maendeleo katika sehemu tofauti tofauti duniani.

Jambo hili limechangia kwa wingi ubunifu wa sera za kiuchumi ambazo haziambatani na hali ilivyo barani. Matokeo ni uchumi ambao unawanufaisha wachache na kuwaangamiza wengi. Sera hizi zimeenziwa kwa muda mrefu na taasisi mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo Benki ya Dunia.

Asilimia kubwa ya historia kuhusu Afrika haijanakiliwa jinsi ipasavyo na kasumba hii ilifanywa kimakusudi. Kwa mfano, itakuaje kwamba mandhari mengi barani Afrika – milima, mito, ziwa – yana majina ya kizungu? Isitoshe, kasumba nyingine inayoudhi ni dhana potovu kwamba wazungu ndio waliogundua mandhari haya!

Je, kuna matumaini yoyote kuhusu jinsi ambavyo Afrika inaweza kujikwamua kutoka kwa ukoloni mamboleo? Kwa sasa ni vigumu mno kwani si Waafrika wengi wanapania kuzungumza peupe kuhusu kasumba hii. Vitu viwili ni muhimu. Kwanza, mfumo wa uongozi wa kisiasa unafaa uzingatie ukoloni mamboleo kama tishio kubwa kwa uhuru halisi wa Waafrika. Pili, mitaala ya elimu sharti ibadilishwe na inakiliwe kwa njia inayowezesha uhuru wa kiakili.

 

Mwandishi ni mchumi wa kisiasa na mshauri wa maswala ya utawala, kanda-siasa na sera za umma. Mitandao ya kijamii: Twitter: @SitatiWasilwa; Facebook: Sitati Wasilwa; LinkedIn: Sitati Wasilwa.

 

 

 

Suggested reads:

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Open chat
1
Need help?
Writers Guild Kenya
Hello.
How can we help you?